Mwingira afunguka kummaliza Babu wa Loliondo

Jumatatu , 8th Apr , 2019

Mchungaji wa Kanisa la Efatha Ministry lililopo Jijini Dar es salaam, Josephat Mwingira, amefunguka jinsi alivyommaliza Babu wa Loliondo na kikombe chake, ambacho alidai kuoteshwa na Mungu.

Akizungumza kwenye ibada ya Jumapili ya Aprili 7 2019, Mchungaji Mwingira amesema maombi aliyoyafanya ndiyo yalisababisha kupotea kwa babu wa Loliondo na kikombe chake, kwani alichokuwa akifanya hakikuwa sahihi mbele za Mungu.

Mwingira aendelea kufunguka

Mwingira ameendelea kusema kwamba Mungu hawezi kuzungumza na mtumishi wa Mungu kuhusu kuponya watu kwa miti, kwani Mungu huongea juu ya kunusuru roho za watu, hivyo kama ni kuponya watu kupitia miti, basi ataongea na wataalam wa masuala ya miti ili wafanyie utafiti, ila kwa Mchungaji kutumia miti kuponya ni sawa na uchawi.

“Ikaja ya Loliondo, na yenyewe ikabeba, Mungu haongei na miti, Mungu anaongea na watu, sasa huyu anasema Mungu alinionyesha miti, Mungu akuonyeshe mti badala ya kukuonesha watu!. Mungu hasemi na sisi kuhusu miti, ataongea na madaktari wafanye utafiti kwa miti, sisi tunaongea na roho, miti ya nini!?, pana mgawanyo wa kazi, ukiwa muhubiri anahangaika na miti ni uchawi, na yeye tukamshughulikia”, amesema Mwingira.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2011 Mchungaji Mstaafu wa kanisa la Kilutheri Tanzania, Ambilikile Mwasapile, alisema kuwa ameoteshwa na Mungu mti wa kutibu magonjwa mbali mbali ikiwemo Ukimwi, na kukusanya maelfu ya watu alkitibu kwa shilingi 500, huku mamia ya watu wakipoteza maisha wakiwa njiani kwenda nyumbani kwake Loliondo kupata tiba.

Hivi sasa mchungaji huyo haendelei na tiba hiyo, lakini alifanikiwa kukusanya pesa nyingi kutokana na maelfu ya watu waliokwenda, na pia serikali iliweza kupeleka huduma za kijamii kwa haraka katika eneo hilo lililopo mkoa wa Arusha.

Mchungaji Mwingira