Jumapili , 7th Apr , 2019

Kampuni ya uchimbaji madini ya Ghuanshan International inayomilikiwa na Wachina nchini Kenya, imezua mtafaruku baada ya kupeleka msaada wa bia eneo la Tiaty, ambao wamekumbwa na balaa la njaa.

Kampuni hiyo ambayo iliamua kuunga mkono jitihada za kunusuru jamii zilizokumbwa na uhaba wa chakula kutokana na ukame, kwa kwenda kuwapa msaada wa vyakula mbali mbali zikiwemo na bia, jambo ambalo limeleta mtafaruku mkubwa nchini Kenya.

Wakati msaada huo ukitolewa katika eneo la shule ya Katikit iliyopo Tiaty, wazee na watoto walikuwa wakitazama, huku vijana wakigombania misaada hiyo.

Wachina wakitoa misaada

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Khan Ke amesema kwamba waliamua kuweka na bia kwenye vyakula walivyowapelekea, baada ya kugundua kuwa wakazi hao pia wanapenda bia.

Hata hivyo wataalamu wa afya waliingilia kati wakisema kuwa jambo hilo sio sahihi, akiwemo Mkurugenzi wa Afya nchini humo Dkt. Kepha Ombacho, ambaye amesema si sawa kiafya kupeka bia kwatu ambao wana njaa, kwani tumbo lisilo na kitu likikutana na pombe hufanya kazi kwa haraka sana na mwishowe huleta madhara.

Hata hivyo wakazi wa maeneo hayo wameonekana kufurahia misaada hiyo ikiwemo pombe, kwani walionekana wakigombania na wengine kukimbia nazo kwenda kuhifadhi nyumbani.