Nyoka weusi wakutwa ofisini kwa Rais

Jumamosi , 20th Apr , 2019

Nyoka wawili wamepatikana katika ofisi ya rais wa Liberia George Weah , hatua iliomshinikiza kuondoka katika ofisi yake na kufanya kazi nyumbani.

Taarifa kutoka kwa katibu wa masuala ya habari Smith Toby, zinasema kuwa nyoka hao ambao ni weusi walipatikana katika jengo la ofisi ya wizara ya maswala ya kigeni, na wafanyikazi wote kutakiwa kutoingia katika ofisi hiyo.

Jinsi nyoka walivyoonekana

 

''Wizara ya maswala ya kigeni ndio ilio na ofisi ya rais, hivyo basi ikalazimika kuandika barua ikiwasihi wafanyakazi kubaki nyumbani huku wakiendelea kuweka dawa,'' amesema Bwana Toby 

''Nyoka hao hawakuuliwa, kulikuwa na shimo mahali fulani ambalo walitumia kurudi''. Aliendelea kuelezea bwana Toby

Video iliochapishwa katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la African News ilionyesha wafanyakazi wakijaribu kushambulia nyoka wakati walipoonekana katika eneo la kukaribisha wageni la jengo hilo.

Maafisa wa polisi na maafisa wa usalama wa rais walionekana wakiyalinda makao ya bwana Weah katika mji mkuu wa Monrovia, na kwamba Rais Weah anatarajiwa kurudi ofisini siku ya Jumatatu.