Orodha ya simu zitakazofungiwa Whatsapp

Jumatano , 2nd Jan , 2019

Wamiliki wa simu zinazotumia programu endeshi ya simu aina ya Series 40 wamekuwa hawawezi tena kutumia mtandao wa WhatsApp kwenye simu zao.

Pichani, simu yenye programu ya 'Whatsapp'.

Hiyo imetokana na uamuzi wa kampuni ya Facebook inayomiliki mtandao wa kijamii wa WhatsApp kuacha kutengeneza app yake kwa njia ambayo inaweza kutumiwa katika simu hizo.

Watu wengi zaidi wataathirika katika kipindi cha mwaka ujao, 1 Februari, 2020 ambapo simu nyingi zikiwemo baadhi ya iPhone zitapoteza uwezo wa kutumia WhatsApp.

Hata kabla ya wakati huo kufika, Facebook wameonya kwamba, "kwa sababu hatutakuwa tukitengeneza na kuboresha app yetu tukizizingatia, huenda baadhi ya uwezo wake ukaathirika wakati wowote".

Zitakazoathirika mwaka ujao ni za Android zinazotumia Android 2.3.7 na miundo ya awali, pamoja na iPhone zinazotumia iPhone iOS 7 na zile za chini ya hapo. Kwa sasa, mfumo huo wa Android umefikia 9.0.

Wanaotumia Android 2.3.7 kwenda nyuma hawawezi kufungua akaunti mpya za WhatsApp, ili uweze kutumia mtandao huo kwa sasa unahitajika kuwa unatumia Android 2.3.3 kwenda juu na Windows Phone 8.1 kwenda juu.

Kwa sasa, walioathirika zaidi ni wanaotumia baadhi ya simu za Nokia zinazotumia mfumo endeshi wa Series 40 ambao wakati mwingine huitwa S 40 OS. Miongoni mwa simu maarufu zilizoathirika ni Nokia 6300.