''Rais Magufuli ni mkali sana'' - Wahadzabe

Jumanne , 18th Jun , 2019

Baada ya muda mrefu, hatimaye Jamii ndogo ya kabila la Wahadzabe ambao kwa asili husishi mapangoni na chini ya mibuyu mikubwa imeanza kutambua umuhimu wa watoto wao kupata elimu.

Baadhi ya wanajamii wa kabila la Wahadzabe

www.eatv.tv kupitia kwa mwandishi wake Dotto Kadoshi, imewatembelea wananchi hao waishio katika Bonde la Eyasi wilayani Karatu mkoani Arusha ambapo wameeleza kuwa wameelewa kuwa elimu itawasaidia, kukabiliana vyema na mabadiliko ya tabia nchi ambayo tayari yameonekana kuanza kuathiri mfumo mzima wa maisha yao ya asili.

Jamii hiyo ambayo kwa asili, pamoja na kuishi mapangoni au chini ya mibuyu mikubwa lakini pia huendesha maisha yao kwa kuwinda, kuokota matunda, kuchimba mizizi porini na kula nyama mbichi hususani ya nyani, sasa wameanza kubadili mtazamo wao wa kifikra juu ya elimu kwa watoto wao.

Hata hivyo Jamii hiyo imeonesha wasiwasi wake wa kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yake ya asili ya kila siku kutokana na kuingiliwa maeneo yao na baadhi ya jamii nyingine.

Asili ya Jamii ya kabila la Wahadzabe inaelezwa ni Afrika Kusini, ambapo katika harakati zao za uwindaji na kusaka matunda maelfu ya miaka iliyopita waliingia Tanganyika kupitia misitu ya Kongo.