Jumatano , 8th Nov , 2023

Siku ya jana Novemba 08, 2023 kampeni ya Namthamini ilifika katika mkoa wa Mara na kugawa taulo za kike katika wilaya mbili za Musoma na Butiama katika shule mbili za sekondari Mwisenge (Musoma) na Kyanyari (Butiama).

Balozi wa kampeni ya Namthamini, Justine Kessy akikabidhi taulo za kike kwa mwanafunzi wa shule ya Sekondari Kyanyari iliyopo Butiama, Mara

Kampeni ya Namthamini ilianza na wanafunzi wa shule ya msingi ya watoto wenye ulemavu Mwisenge iliyopo wilaya ya Musoma mkoani Mara ambao walipatiwa taulo za kike ambazo zitaweza kuwasadia wanafunzi 400 wa kike kwa mwaka mzima.

Kisha ikaelekea katika wilaya ya Butiama katika shule ya Sekondari Kyanyari ambapo zilitolewa taulo za kike zenye uwezo wa kuwasaidia wanafunzi 400 kwa kipindi cha mwaka mzima.

Mbali na kupatiwa taulo za kike wanafunzi wa shule hiyo walipatiwa elimu ya hedhi salama na kujengewa uwezo wa kujiamini wanapokuwa kwenye kipindi cha hedhi.

Lucia Masinde mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari Kyanyari anasema kabla ya kupata elimu ya hedhi salama kupitia kampeni ya Namthamini wanafunzi walikuwa hawashirikiani wanapokuwa kwenye kipindi cha hedhi na wanafunzi wengine walikuwa wanatumia vitambaa kujistiri kutokana na kukosa uwezo wa kununua pedi.