Jumanne , 7th Aug , 2018

Suala la kutunza nywele za asili wengi hutamani japokuwa ukweli kwamba kuna changamoto kadhaa, lakini kwa mtu aliye makini anao uwezo wa kupata kilicho bora katika nyewle zake. Leo tunaangazia vitu vya kufanya ili kukuza na kutunza nywele za asili.

Kwanza kabisa unapaswa kuzikubali nywele zako na kuzipenda , jambo hilo litapelekea mahusiano mazuri, kuelewa tatizo la nywele zako na kuanza kuchukua hatua taratibu ya kuzipatia uvumbuzi tatizo hilo.

Pili, unapaswa kufanya usafi wa kina wa ngozi na nywele zenyewe kwasababu endapo nywele zitaachwa chafu, basi ule uchafu unaziba matundu ya nywele na kuzuia njia kama vile ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata chunusi.

Tatu, ni kulinda unyevu wa nywele . pale zinapooshwa, yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu. Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata kushikilia hayo maji yaliyoo vizuri na zikikauka zinakuwa kavu sana. Ni vizuri kabla hazijakauka vizuri, zikafanyiwa ‘condition’ , kwa zile nywele ambazo ni nyepesi na chache pia kuna bidhaa zinasaidia kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

Hatua nyingine ni ya kupaka mafuta kichwani, kwani mafuta yana umuhimu mno katika ukuaji wa nywele na mafuta mazuri ni ya nazi ambayo yamewafaa baadhi ya watumiaji wengi .

Njia nyingine ni ya kuzichambua vizuri nyele kabla ya kuzichana, hapa mtu anatakiwa kuwa na subira na nywele zake , asifanye pupa kuzichana na ikiwezekana aziloweshe maji kidogo halafu ndipo azichane kwa chanuo kubwa lenye upana wa kutosha (wide toothed comb) ili kuzipa afya na kuepuka kujiumiza wakati wa kuzichana.

Pia mtu anayetunza nywele za asili anatakiwa kupunguza matumizi ya vitu vyenye moto katika nywele zake kama vile pasi ya nywele na vingine kama hivyo. Nywele zinatakiwa zichanwe kawaida na ziachwe zikauke zenyewe kwa hewa bila kuzilazimisha.