Jumatano , 16th Aug , 2017

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeahirisha kesi ya kutakatisha fedha na kughushi nyaraka inayowakabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu' hadi Agosti 30 mwaka huu kutokana na upelelezi kutokamilika.

Kesi hiyo imeahirishwa mbele ya Hakimu Victoria Nongwa baada ya Wakili wa upande wa mashitaka kueleza kuwa kwa vile nyaraka za kughushi maandiko zinahitaji utaalam kuzibaini, hivyo kitengo maalum cha kubaini maandishi kinaendelea kufanya uchunguzi ili kukamilisha upelezi huo ambapo aliomba kesi hiyo isogezwe mbele kwa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi.

Hakimu Victoria Nongwa aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha haraka upelezi wao ili kesi hiyo ianze kusikilizwa ambapo aliisogeza hadi Agosti 30 ili kuwapa nafasi kukamilisha upelelezi wao huku watuhumiwa wakirudishwa gerezani.

Aveva na Kaburu wanashtakiwa na TAKUKURU wakikabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka za Klabu ya Simba na kutakatisha dola za Marekani 300,000 (zaidi ya Sh milioni 650) na wamekuwa rumande tangu Juni 29, mwaka huku wakiwa na safari za kwenda na kurudi mahakamani kwa kile kinachodaiwa kuwa upelelezi haujakamilika