Ijumaa , 19th Dec , 2014

TIMU ya Vijana ya Mkoa wa Dodoma, imefanikiwa kuingia hatua ya Fainali katika michuano ya Copa Cocacola baada ya kuifunga timu kutoka Kigoma goli 2-1, mechi iliyochezwa uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, Kocha wa Timu ya Dodoma, Mussa Furutuni amesema mechi hiyo ilikuwa na changamoto nyingi pamoja na ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuhitaji kupata ushindi ili iweze kufika hatua ya fainali na hatimaye kuibuka na ushindi.

Furutuni amesema japo ni mara ya kwanza kwa vijana wake kuingia hatua hiyo ya fainali lakini siri kubwa ya kuweza kufanya vizuri katika mashindano ni maandalizi mazuri ikiwemo na mazoezi pamoja na nidhamu ya kimchezo.

Kwa upande wake, Kocha kutoka Mkoa wa Kigoma, Hamis Mabo amesema mchezo ulikuwa mgumu kutokana na kila timu kutumia uwezo wake ili kuweza kuibuka na ushindi lakini kutokana na makosa ya kimchezo yalipelekea timu yake kupoteza mchezo huo.