Alichokifanya Tulia Ackson kuelekea 'Yes We Can'

Ijumaa , 11th Jan , 2019

Baada ya taarifa ya klabu ya Simba iliyotolewa jana ikieleza kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya JS Saoura ni Naibu Spika Tulia Ackson, naye ameitikia na kuwataka Watanzania wafike uwanjani kwa wingi.

Naibu Spika Tulia Ackson

Tulia amesema kwa kuwa Simba ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa ni lazima kuwaunga mkono ili wafanye vizuri na kulitoa kimasomaso taifa.

''Watanzania tukutane uwanja wa Taifa siku ya Jumamosi, kuwapa hamasa wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Africa Simba SC Tanzania, nguvu yetu mashabiki ndio ushindi wa timu yetu'', amesema.

Tayari wapinzani hao wa Simba wametua nchini kutoka Algeria usiku wa jana, na leo watafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Taifa ili kujiweka sawa na mchezo huo.

Simba ipo kundi D na timu za Al Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria na AS Vita Club ya DR Congo. Vita Club kesho itakuwa ugenini Misri kucheza na Al Ahly.