Ijumaa , 23rd Apr , 2021

Mcheza kikapu nyota wa timu ya Los Angeles Lakers, Anthony Davis amerejea dimbani alfajiri ya leo wakati timu yake iliponyukwa na Dallas Mavericks kwa alama 115-110 ikiwa ni kwa mara ya kwanza tokea nyota huyo akosekana uwanjani tokea Februari 23, 2021.

Nyota wa Los Angeles Lakers, Anthony Davis.

Davis ambaye ameondoka  na alama 4, rebaundi 4 na Assisti 1 ndani ya dakika 16 alizocheza, amesema kukosa kwake michezo 30 ya ligi kuu ya kikapu nchini Marekani ‘NBA’ msimu huu, kulichangiwa na maumivu ya misuli yaliyompa hofu kubwa na kumfanya achelewe kurejea.

Baada ya Davis kurejea, kocha wake Frank Vogel amesema, alipanga kumchezesha nyota huyo dakika 15 za kumpiga jeramba imsaidie awe fiti kuelekea michezo mingine inayofuata ambayo ni muhimu kwa Mabingw hao watetezi kwenye kutetea kombe lake.

Licha ya Davis kurejea, lakini Lakers wataendelea kumkosa nyota wake mwingine, Lebron James kwa takribani majuma mawili baada ya nyota huyo kupata maumivu ya kifundo cha mguu.

Lakers kwasasa ipo nafasi ya 5 kwenye msimamo wa NBA kwenye upande wa Magharibi huku ikiwa na mwendo wa kusua sua kujikwamua kwenye nafasi za michezo ya mtoano ilhali wakitegemea kushuka tena dimbani dhidi ya wababe wao Dallas Mavericks Aprili 24, 2021.

NBA inatazamiwa kuendelea usiku wa kuamkia kesho kwa michezo 9, huku ile inayotazamiwa kuwa yenye msisimko mkubwa ni pamoja na:

Brooklyn Nets itakayocheza saa 8:30 usiku dhidi ya Boston Celtics bila Kevin Durrant na James Harden  huku Milwaukee Bucks ikitaraji kucheza na vinara wa NBA upande wa Mashariki Philadelphia 76ers saa 4:30 usiku wa kesho.