Jumatatu , 24th Sep , 2018

Mlinda mlango wa Arsenal, Petr Cech amesema klabu hiyo imepoteza hali ya ushindi kutokana na kutoshinda mataji kwa kipindi kirefu.

Mlinda mlango, Petr Cech

Arsenal ilishinda taji lake la mwisho la ligi kuu nchini Uingereza, EPL msimu wa 2003/04 na haijafanikiwa kufuzu michuano ya Klabu bingwa Ulaya kwa misimu miwili ya mwisho, jambo ambalo Cech anaamini linaifanya klabu hiyo isahau namna ya kushinda mataji.

Cech ana mataji manne ya EPL, ambapo yote ameshinda akiwa na klabu ya Chelsea kabla ya kujiunga na Arsenal mwaka 2015.

“ Kwa klabu yoyote ambayo inashinda vikombe katika miaka ya karibuni inakuwa na kikosi ambacho kinajua namna ya kushinda mechi zao na mataji, hilo unaweza ukaliona wazi uwanjani ”, amesema Cech.

“ Inachukua muda kama Tiger Wood ambaye amechukua miaka mitano bila kushinda taji lolote kubwa, na kadri miaka inavyoongezeka na ugumu unavyozidi kuongezeka pia. Klabu hii haijashinda ubingwa kwa miaka 10 sasa, kwahiyo inabidi turudi nyuma tufahamu namna gani ya kushinda ”, ameongeza Cech.

Mchezo uliopita wa EPL ulikuwa bora sana kwa Petr Cech ambaye mara kadhaa amekuwa akilaumiwa kwa udhaifu katika miguu yake, aliisaidia Arsenal kushinda mchezo wake wa tano mfululizo katika mashindano yote baada ya kupoteza mechi mbili za awali za ligi.

 Golikipa huyo anaamini kuwa Arsenal itashinda mataji baada ya muda mfupi kutokana na maendeleo anayoyaona kupitia kwa kocha wake mpya, Unai Emery ambaye wameanza naye tangu msimu ulipoanza.

“ Tunafanya kazi, tunajaribu kufanya kila namna na kukusanya alama kadri inavyowezekana huku tukiendelea kuwa bora katika kila mchezo. Tuna furaha na alama tunazozipata  ”.