Jumamosi , 1st Aug , 2015

Klabu ya soka ya Azam fc ya Tanzania kesho inaingia katika fainali ya kombe la klabu bingwa ikiwa na hamu ya kuweka rekodi mpya kwa timu hiyo ambayo imetinga fainali hiyo kwa kishindo baada ya kushinda michezo yake yote ya hatua zilizopita.

Kikosi cha Azam FC ambacho kitavaana na Gor Mahia.

Kesho ndio kesho nyasi za uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam zitakuwa zikiwaka moto wakati mashabiki wa soka nchini wakishuhudia mtanange wa fainali ya michuano ya klabu bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati [maarufu kombe Kagame] ikihusisha miamba miwili ya soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati timu za Azam fc ya Tanzania inayonolewa na kocha Muingereza Stewart Hall aliyewahi kuifikisha fainali za Kagame mwaka 2012 na Gor Mahia iliyo chini ya kocha Mscoch, Frank Nuttal wakionyeshana kazi.

Mchezo huo wa fainali kati ya Azam fc na Gor Mahia utatanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu baina ya Al Khartoum na KCCA ambao watavaana muda mchana.

Afisa habari wa Azam FC Jafar Idd Maganga amesema ni wazi kesho patachimbika, kila timu ikitaka kutibua rekodi ya mwenzake na kutaka kuweka rekodi mpya, ambapo Azam ikitaka taji la kwanza la michuano hiyo huku pia Gor Mahia nao wakisaka taji la kwanza baada ya miaka 30.

Gor pia inashikilia rekodi ya kucheza mechi mfululizo mwaka huu bila kupoteza, ikiwa imefikisha 24, zikiwamo 18 za Ligi Kuu Kenya wanayoiongoza na sita za Kombe la Kagame.

Gor ilifika fainali na kunyakua taji mwaka 1985 (wakati huo klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati) na kesho itakuwa nafasi yao ikiwa chini ya Kocha Mscoch, Frank Nuttal.

Mbali na timu hizo kuwa katika vita ya kuwania rekodi mpya, pia kutakuwa na mchuano mkali wa kuwania Kiatu cha Dhahabu kati ya mastraika Michael Olunga wa Gor mwenye mabao matano na Kipre Tchetche wa Azam mwenye mabao matatu.

Wachezaji hao wanatengenishwa na Salah Bilal wa Al Khartoum mwenye mabao manne ambaye naye atakuwa vitani dhidi ya KCCA kusaka nafasi ya tatu katika mechi itakayoanza saa nane.