Ijumaa , 20th Jul , 2018

klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imekuwa timu ya pili kufuata nyayo za mabingwa watetezi wa ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC kutangaza mipango yao kuweka kambi nje ya nchi kuelekea michuano ya ligi kuu inayotarajiwa kuanza Agosti 22, mwaka huu.

Azam FC iliyopo juu kwenye picha huku Simba yenyewe ikiwa kwa chini

Hayo yamebainishwa na Afisa habari wa klabu hiyo, Jaffer Idd Maganga na kusema kwamba lengo kubwa ya safari hiyo ni kutaka kumpa fursa kocha wao mpya Hans Pluijm kuwajua vizuri wachezaji na kuipangilia vizuri timu ili kusudi watakaporejea nchini Agosti 15 wawe tayari wameshajuana vizuri.

"Klabu ya Azam inatarajia kuondoka nchini kuelekea Uganda mnamo Julai 30, ina kwenda huko kwaajili ya mazoezi pamoja na kucheza mechi mbalimbali za kirafiki nchini humo na tunatarajia kurejea Agosti 15", amesema Maganga.

Pamoja na hayo, Maganga ameendelea kwa kusema "safari hii itampa fursa mwalimu Hans kuwajua wachezaji ambao anawafundisha maana hajawahi kukaa nao na vile vile kuweza kutengeneza timu yenye umoja na ushirikiano ambayo itakuja kupambana kwenye ligi kuu na kwa jinsi tulivyosajili basi tunaamini tutapata mafanikio makubwa".

Katika timu zinazoshiriki michuano ya ligi kuu Tanzania Bara, Azam Fc imekuwa ya pili kufuata nyayo za Simba SC kuweka mipango yake hadharani ya eneo ambalo watakuwa wanajifua kuelekea michuano hiyo.

Msimu ulioisha wa ligi kuu Tanzania bara 2017/18, Azam FC ili maliza ligi ikiwa nafasi ya pili kwa alama 58 akifuatiwa na Yanga SC ambaye alikuwa bingwa mtetezi kwa alama 52 huku Simba akishika na nafasi ya kwanza kwa alama 69.