Jumatano , 24th Jan , 2018

Klabu ya Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imesema itafanya kila namna ili iweze kupata ushindi katika mechi yake dhidi ya Yanga SC siku ya Jumamosi, japokuwa wanaifahamu ubora na ukubwa wa timu hiyo.

Kikosi cha Klabu ya Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC

Hayo yameelezwa na Afisa Habari wa Klabu hiyo Jaffar Iddy Maganga wakati alipokuwa anazungumza na  waandishi wa habari mchana wa leo Jijini Dar es Salaam kuhusiana na mchezo huo ambao umepangwa kufanyika majira ya saa 1:00 usiku katika viunga vya Azam Complex nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

"Sisi kama 'Azam Football Club' tunafahamu umahiri wa timu ya Yanga SC na ukubwa wake lakini huu ni mchezo wa mpira. Mchezo wa mpira maana yake endapo utajiandaa vizuri utaweza kufanya vizuri pia. Mechi ya Jumamosi itakuwa na ushindani wa hali ya juu lakini tunajipanga vizuri ili twende kupambana", alisema Jaffar Maganga.

Pamoja na hayo, Jaffar Maganga ameendelea kwa kusema "mchezo wa mpira una matokeo matatu ambayo ni kushinda, kufungwa na sare hayo ndio matokeo ya uwanjani na dakika 90 lazima zitumike katika matokeo haya. Timu ipo vizuri na imebadilika safari hii mwalimu atawatumia vijana ili waweze kufahamika na watambue namna ya kupambana katika michuano ya  Ligi Kuu Tanzania Bara"

Kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga.

Kwa upande mwingine Afisa habari huyo amesema watatumia mchezo huo dhidi ya Yanga SC kuweza kurudi katika nafasi yao ya kuongoza Ligi Kuu kama ilivyokuwa hapo awali.

"Kisoka tunahitaji tupate ushindi ili tukae sawa kwa maana tumepitwa na Simba, na sasa hivi wapo mbele kwa alama 2 kwa hiyo ni umbali mkubwa kimpira, awali tulikuwa tunashindana nao, kukimbizana kwa pointi sawa lakini tukitofautina kwa magoli", alisisitiza Jaffar Maganga.