Jumatatu , 16th Sep , 2019

Kocha wa klabu ya Triangle United, Taurai Mangwilo ametaja kitu kimoja kikubwa ambacho anajivunia katika klabu yake na kitakachowasaidia kusonga mbele kwenye mchezo wa marudiano.

Mchezo wa Azam FC dhidi ya Triangle United

Katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho uliofanyika Jumapili, Septemba 15 Jijini Dar es Salaam, Azam FC imepoteza kwa bao 1-0, huku bao hilo pekee la Triangle likifungwa na Ralph Kawondera katika dakika ya 34.

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Triangle amesema kuwa kitu pekee wanachojivunia ni rekodi yao ya kutopoteza mchezo wowote ambao wanakuwa wa kwanza kupata bao.

"Sisi kama timu hatujawahi kupoteza mchezo wowote ambao tumetangulia kupata bao, kwahiyo matarajio yalikuwepo kwenye mchezo ule. Tulijaribu kuwasukuma ili tupate bao na tulipolipata tukajiamini kuwa tayari tuna kitu kikubwa sana", amesema Mangwilo.

Azam FC inatarajia kusafiri hadi nchini Zimbabwe kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Triangle, ambapo inahitaji kushinda ugenini kwa idadi ya mabao mawili au zaidi ili iweze kusonga mbele katika hatua ya makundi ya michuano hiyo.