Baada ya kichapo, Manara aja kivingine

Jumapili , 10th Mar , 2019

Kufuatia Simba kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa JS Saoura Februari 9 nchini Algeria, Afisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara amezungumzia hatma yao katika michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika.

Haji Manara akiwa ameinama kwenye moja ya mchezo katika uwanja wa taifa.

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo, Manara aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram akisema kuwa kwao mapambano bado yanaendelea na wanayo nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa ya vilabu barani Afrika.

"Ni Do or Die Match. Ni zaidi ya kufa au kupona Kwenye mchezo wetu wa mwisho dhidi ya AS Vita utakaochezwa Taifa, Jumamosi ijayo!!, bila kujali matokeo yatakayotokea Egypt baina ya Al Ahly na Soura ambao nao wanacheza siku hyo ya tarehe 16", amesema Manara.

"Ushindi wowote tutakaoupata dhidi ya Wacongo hao tutafuzu katika robo fainali!!. Hiyo sio 'Yes We Can', hiyo ni 'Do or Die' kama ilivyokuwa na Nkana, Insha'Allah itakuwa", amemalizia Manara katika ujumbe huo.

Kabla ya mchezo wa Simba hapo Jumamosi, ulitanguliwa na mchezo wa AS Vita Club walioikaribisha Al Ahly mjini Kinshasa, ambapo mchezo huo ulimalizika kwa AS Vita kuibuka na ushindi wa bao 1-0, bao lililofungwa katika na Tuisila Kisinda katika dakika ya 84'.

Baada ya matokeo ya michezo hiyo, sasa kundi D linaongozwa na JS Saoura yenye pointi 8 ikifuatiwa na Al Ahly na AS Vita Club zenye pointi 7 huku Simba ikiwa mkiani kwa pointi 6. Mpaka sasa timu yoyote katika kundi hilo inaweza kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali endapo itashinda katika mchezo wa mwisho.

Hata hivyo baada ya kumalizika kwa mchezo wa JS Saoura na Simba, mashabiki na wadau wa soka nchini Tanzania wameonesha kutoridhishwa na kiwango cha beki, Paul Bukaba kutokana na kufanya makosa kadhaa ambayo yalipelekea kuadhibiwa kwa mkwaju wa penalti.

Kuelekea mchezo wa mwisho dhidi ya AS Vita Club katika uwanja wa taifa wikiendi hii, Manara amesema kuwa kutokana na ukubwa wa klabu ya Simba na wingi wa mashabiki, uwanja huo unahitajika kuongezwa.

"People’s Club!, ( klabu ya watu ) na ndio inaongoza kujaza uwanja Afrika nzima kwenye CL!!. Ipo hoja na haja ya kuupanua uwanja mkuu wa Taifa ( huku sisi tukianza kujenga wetu) kwa sababu Simba tupo wengi, uwanja wa Taifa haututoshi ", amesema.