Jumapili , 28th Jan , 2018

Baada ya kupoteza mchezo wake wa raundi ya 15 wa ligi kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC, klabu ya Azam FC imesafiri kuelekea Morogoro kwaajili ya mchezo wa kombe la shirikisho.

Azam FC ilipoteza kwa mabao 2-1 licha ya kutangulia kwa bao la mapema, lakini Yanga ilitokea nyuma na kusawazisha kabla ya kuongeza bao la pili katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Azam Complex.

Msemaji wa timu hiyo Jaffary Idd amesema kikosi cha Azam FC kinatarajia kuelekea mkoani Morogoro leo mchana kwaajili ya mchezo wake wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Shupavu FC.

Mchezo huo ni wa raundi ya tatu ya kombe hilo ambalo bingwa wake huwa anapata nafasi ya kuliwakilisha taifa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Bingwa wa msimu uliopita ni Simba SC ambaye ndiye anawakilisha taifa msimu huu.

Shupavu FC dhidi ya Azam FC zitakutana siku ya Jumanne Januari 30, kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro saa 8:00 Mchana.