Jumanne , 14th Jun , 2016

Chama cha mchezo wa mbio za baiskeli nchini Tanzania CHABATA kimesema msimu huu kimejipanga kuhakikisha wanashiriki mbio zote zilizosalia ambazo zitafanyika kuanzia mwezi Julai na baadae mwishoni mwa mwaka huu.

Baadhi ya waendesha baiskeli wakichuana.

Mwenyekiti wa chama cha baiskeli nchini Tanzania CHABATA Geofrey Mhagama amesema mwaka huu watashiriki mashindano mawili makubwa ya kimataifa ya mbio za baiskeli za Tour De Congo na ile ya Tour de Rwanda pamoja na kuwa wanajukumu la michuano ya ubingwa wa taifa mbele yao.

Mhagama amesema katika kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kukuza mchezo huo wameanza mkakati wa kuhakikisha kila eneo ambalo liko hai [active] katika mchezo wa baiskeli basi linakuwa likifanya mashindano ya mara kwa mara hata kama ni madogo kwa lengo la kuibua na kupata wachezaji wazoefu wa mchezo huo na wenye vipaji ambao baadae wataunda kombaini za maeneo yao kwaajili ya kushiriki mashindano ya ngazi za juu zaidi.

Aidha Mhagama amesema pamoja na ratiba ya michuano ya mbio za Toure de Congo kuonekana iko karibu na mashindano ya ubingwa wa taifa wa Tanzania hivyo kutishia ushiriki wa nchi katika michuano hiyo ya kimataifa wao kama chama wakishirikiana na mdhamini waliyempata wanataraji kuweka wazi tarehe rasmi ya kucheza michuano ya taifa kulingana na michuano hiyo na kama itaonekana kuingiliana basi wataahirisha ya taifa na hivyo kulazimika kutumia wachezaji wa kikosi cha zamani cha timu ya taifa ambao watashindaniswa na nyota wachache wa mikoani ili kupata washiriki wa dharula wa michuano hiyo ya Congo.

Akimalizia Mhagama ametoa wito kwa viongozi wa mchezo baiskeli kuanzia ngazi ya vitongoji, tarafa, wilaya na mikoa kuanzisha mashindano mengi ya mchezo huo katika maeneo yao kwajili ya kuibua vipaji na kupata wachezaji bora ambao watakuwa na uzoefu wa kushindana na hatimaye kushiriki mashindano ya taifa ili kupata kikosi bora kitakachoteuliwak kuunda timu ya taifa itakayoshiriki michuano mbalimbali ya kimataifa.