Jumatatu , 15th Jan , 2018

Nyota wa Barcelona Lionel Messi amevunja rekodi iliyodumu kwa miaka 54 na kuweka rekodi yake mpya ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye ligi moja na klabu moja.

Messi amefanikiwa kuvunja rekodi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na nyota wa zamani wa Bayern Munich Gerd Muller, baada ya jana usiku kufunga bao moja na la nne kwenye ushindi wa mabao 4-2 iliopata Barcelona dhidi ya Real Sociedad.

Baada ya kufunga jana Messi amefikisha mabao 366 huku bao moja kati ya hayo amewahi kufunga kwa mkono, hivyo kuwa mchezaji mwenye mabao mengi kwenye ligi tano bora barani Ulaya ndani ya klabu moja.

Gerd Muller alikuwa akishikilia rekodi hiyo ya kufunga mabao 365 aliyoiweka akiwa mchezaji wa klabu ya Bayern Munich kwenye miaka ya 1964 na 1979.

Muller alifunga mabao 365 ndani ya mechi 427 za ligi kuu ya soka Ujerumani Bundesliga na Messi amefunga mabao 366 ndani ya mechi 401 alizoichezea Barcelona kwenye La Liga.

Katika rekodi hiyo Messi amefunga mabao 288 kwa mguu wa kushoto, 64 mguu wa kulia, 13 kwa kichwa na bao moja kwa mkono alilofunga Juni 09 mwaka 2007 dhidi ya Espanyol.