
Taifa stars itacheza mchezo wake wa pili wa kundi D kwenye michuano ya CHAN, dhidi ya Namibia kesho Januari 23, 2021
Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kitashuka tena dimbani kesho Jumamosi Januari 23, 2021. ambapo kitaminyana na timu ya taifa ya Namibia mchezo utakao chezwa saa 4:00 usiku kwa Saa za hapa nyumbani.
Sasa kuelekea mchezo huo wa kesho Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la soka hapa nchini TFF ambaye yupo na kikosi cha stars huko nchini Cameroon amesema
“kiukweli nia ni kupata ushindi ama matokeo chanya katika mchezo unaokuja dhidi ya Namibia, na tunafahamu ni mchezo ambao kwetu ni kama fainali na hata mchezo ambao utabakia dhidi ya Guinea nao ni kama fainali kuhakikisha kwamba katika kundi D, basi tunakuwa ni moja kati ya timu ambazo zinatoka katika kundi letu kuelekea katika hatua ambazo zinafuata hilo ndio lengo katika mashindano haya ambayo tupo hapa nchini Cameroon”
Mshambuliaji wa taifa stars John Bocco kushoto, na mlinzi Ibrahim Ame kulia wameanza mazoezi baada ya kuwa nje kutokana na majeruhi
Taifa stars ilipoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa mabao 2-0 na timu ya taifa ya Zambia, na sasa kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mrundi Etienne Ndayiragije kinahitaji kupata matokeo ya ushindi ili kufufua matumaini ya kusonga mbele katika hatua inayofata.
Kuhusu hali ya kikosi ndimbo ameweka wazi kuwa wachezaji wenye majeruhi John Bocco na Ibrahim Ame wameaza mazoezi na watasubiri ripoti ya mwisho ya madaktari kabla ya mchezo ili kujua nafasi yao kwenye mchezo dhidi ya Namibia.