Jumamosi , 6th Jan , 2018

Baada ya kukaimu nafasi ya unahodha wa kikosi cha Simba SC kwa miezi kadhaa leo rasmi mshambuliaji John Bocco ameteuliwa kuwa nahodha kamili wa vinara hao wa ligi kuu soka Tanzania Bara.

Uteuzi huo umefanywa na kocha msaidizi wa Simba Masoud Djumaa Irambona, na kupewa baraka na uongozi wa klabu hiyo. Bocco anachukua nafasi iliyokuwa chini ya Method Mwanjali ambaye ametemwa katika usajili wa dirisha dogo.

Masoud pia amemthibitisha beki wa kushoto wa klabu hiyo na mchezaji bora wa ligi msimu uliopita Mohammed Hussein, kuwa nahodha msaidizi wa klabu hiyo. Kiungo Mkongwe wa klabu hiyo Mwinyi Kazimoto yeye atakuwa nahodha namba tatu.

John Bocco amejiunga na Simba msimu huu akitokea klabu ya soka ya Azam FC ambayo ameichezea takribani miaka 10. Bocco alipanda daraja na Azam FC mwaka 2007 na kuichezea hadi msimu wa 2016/17.

Tangu ajiunge na Simba mshambuliaji huyo amefanikiwa kufunga mabao 6 katika michuano yote. Bocco amefunga mabao matatu kwenye VPL, bao moja kwenye kombe la shirikisho na mabao mawili kombe la Mapinduzi.