Ijumaa , 11th Mar , 2016

Unaweza kusema ni mpambano wa kisasi baina ya mabondia wapinzani wawili kutoka mji mmoja wa Dar es Salaam katika vitongoji tofauti vya Mabibo na Kinondoni kati ya Nasib Ramadhan na Francis Miyeyusho kuwania mkanda wa ubingwa wa kimtaifa wa UBO.

Bondia Nasib Ramadhani wa Tanzania akiwa na moja ya mikanda aliyowahi kushinda.

Bondia wa kimataifa wa ngumi za kulipwa nchini Mtanzania Nasibu Ramadhani wa mabibo jijini Dar es Salaam ameingia kambini rasmi kwa ajili ya kujiwinda na mpambano wa kisasi wa kuwania ubingwa wa kimataifa wa UBO dhidi ya bondia Mtanzania Francis Miyeyusho.

Wakiongea hii leo mara baada ya mazoezi ya kujiwinda na mpambano huo utakaopigwa machi 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam bondia huyo na kocha wake Christopher Mzazi [mzazi respect] wamesema kutokana na mazoezi wanayofanya kwa sasa wanauhakika wakuibuka na ushindi mkubwa.

Nasib ambaye anakutana na Miyeyusho kwa mara ya pili baada ya awali bondia huyo kupoteza mpambano wao wa WBF kwa technical knock out KO kufuatia kuumia sasa anasema yuko fiti kuhakikisha analipa kisasi kwa kumtembezea kichapo kizito mpinzani wake huyo ambaye anamtaja kama bondia ambaye hana uwezo tena wakucheza na damu changa kutokana na umri kumtupa mkono.

Nasib ambaye aliwahi kutwaa tuzo ya bondia bora nchini kutokana na mafanikio aliyoyapata huko nyuma kimataifa pamoja na kutamba ametoa wito kwa mashabiki wake na wapenda michezo wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia akithibitisha kwa vitendo kauli zake za kutoa kichapo kwa mpinzani wake huyo ambaye watakutana naye.