Jumanne , 1st Mar , 2022

Bondia Oleksandr Usyk amejiunga na kikosi cha ulinzi cha Kyiv Territorial Defence kwa ajili ya kuitetea nchi yao na uvamizi unaofanywa na nchi ya Urusi tangu sakata hilo lianze siku ya Alhamisi ya wiki iliyopita.

Bondia Oleksandr Usyk

Usyk mwenye umri wa miaka 35 ambaye ni bingwa wa uzito wa juu duniani akishikilia mikanda kama WBA(Super), IBF, WBO na IBO ameonekana kwenye mitandao ya kijamii akiwa kwenye mavazi ya kijeshi huku akishikilia silaha nzito katika mitaa ya Kyiv, mji ambao unalengwa na Urusi kuweza kuutwaa mpaka sasa.

"Ndugu zangu kutoka Ukraine,watu wengi wameniandika ujumbe kwamba niondoke na kukimbilia sehemu nyingine,sio kweli ,nilikuwa na safari na tayari nimerejea nyumbani na nipo kwangu ,marafiki zangu tunapaswa kuungana kwa pamoja ili kupambana na adui wetu bila kujali itikadi zetu" amesema Usyk

Bondia huyo sasa anaungana na nyota wawili ndugu ambao ni mabondia Wladimir na Vitali Klitschko ambao walijiunga  na jeshi la Ukraine ili kupambana na vikosi vya Urusi huku tayari vikwazo mbalimbali vikizidi kuwekwa kwa Urusi kutoka kwa masharikisho ya michezo kama FIFA,UEFA na IOC kufungia wanamichezo ili kupinga uvamizi wa Urusi kwa Ukraine.