Alhamisi , 18th Feb , 2021

Mshambuliaji hatari wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, Braut Erling Haaland amemwagia sifa na shukrani mshambuliaji wa klabu ya PSG ya nchini Ufaransa, Kylian Mbappe kwa kusema alihamasika kufanya vizuri baada ya kuona amepiga Hat trik dhidi ya Barcelona.

Mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Braut Haaland akishangilia bao baada ya kuwafunga Sevilla usiku wa jana.

Haaland ameyasema hayo baada ya mchezo wa Dortmund kumalizika usiku wa jana na kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Sevilla ya Hispania na yeye akifunga mabao mawili kwenye huo mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya klabu bingwa Barani Ulaya.

Haaland amesema Ninapenda kucheza kwenye usiku wa mabingwa Ulaya na nilihamasika baada ya kuona Mbappe amefunga mabao matatu dhidi ya Barcelona Camp Nou. Ninamshukuru sana Mbappe kwani ulikuwa usiku mzuri kwangu”.

Katika kuzungumzia kiwango cha timu yake baada ya kupata ushini huo kwenye uwanja wa ugenini wa Roman Sanchez Pizjuan, Haaland amesema:

Haikuwa vizuri kwenye kuruhusu mabao 2, lakini ni vizuri kwa kuwa tumefunga mabao 3 ugenini na kuutawala mchezo. Tulikuwa na mpango mzuri kuliko wao”.

Kuelekea kwenye mchezo wa mkondo wa pili tarehe 9 Machi 2021 ili kutafuta atakayetinga hatua inayofuata ya Robo fainali, Haaland amesema;

“Tumefunga mabao 3, lakini tutapaswa kucheza kwa kushambulia sana kwenye mchezo huo. Tunapaswa kuendelea hivyo na kuwa imara zaidi”.

Mpaka kufikia hivi sasa, Haaland ndiye kinara wa kupachika mabao, mabao 8 sawa na jumla ya mabao ambayo Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wamefunga kwenye michuano hiyo hadi sasa.

Kwa uapnde wa michezo ya michuano yote, Haaland amefunga mabao 25 na kutengeneza mengine 7 kwenye michezo 24, ni sawa na kusema amehusika kwenye mabao 32 kwenye michezo 24 kwenye michuano yote.