Alhamisi , 23rd Mei , 2019

Klabu ya soka ya TP Mazembe ya DR Congo, iko mbioni kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.

Ibrahim Ajibu

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TP Mazembe hivi karibuni, imeonesha kuwa timu hiyo inavutiwa na huduma ya Ajibu ambaye pia amewahi kuchezea Simba.

Endapo Ajibu ataungana na klabu hiyo iliyopo chini ya kocha Pamphile Mihayo Kazembe, anaweza kutumika katika maeneo mawili kama mshambuliaji au kiungo mshambuliaji anayecheza nyuma ya washambuliaji.

Endapo atatumika kama mshambuliaji atakutana na changamoto ya washambuliaji wawili wanaoaminiwa kwasasa na kocha Mihayo ambao ni Tresor Mputu na Jackson Muleka.

Kama kocha Mihayo ataamua kumtumia Ajibu kwenye eneo la kiungo mshambuliaji, basi mkali huyo wa pasi za mwisho atakabiliana na changamoto ya viungo kama Elia Meschak, Rainford Kalaba na Abdoulaye Sissoko ambao ndio huwazunguka washambuliaji Tresor Mputu na Jackson Muleka.

TP Mazembe tangu mwaka 2010 imeshafanikiwa kuchukua wachezaji watatu kutoka Ligi kuu soka Tanzania bara ambao ni Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Patrick Ochieng.