Jumatatu , 14th Jan , 2019

Mlinda mlango mahiri wa klabu ya Manchester United, David De Gea amesema hastahili kupewa sifa yeye peke yake kufuatia mchezo wa jana, Januari 13 dhidi ya Tottenham Hotspurs, bali ni kwa timu nzima.

David De Gea

De Gea alikuwa na kiwango chake bora zaidi kuwahi kuonekana tangu mwanzo wa msimu huu, alipowazuia Spurs kusawazisha bao baada ya Man United kutangulia kufunga kupitia kwa Marcus Rashford, bao lililodumu kwa kipindi chote cha dakika 90.

Akizungumza katika Runinga ya klabu hiyo 'MUTV', De Gea amesema, "nilijisikia vizuri baada ya kuokoa michomo miwili, kila mmoja kati yetu aliisaidia timu kuweza kupata 'Cleansheet' na kuisaidia timu kushinda kwahiyo kila mchomo uliookolewa ulikuwa muhimu".

"Victor Lindelof na Phil Jones walikuwa na kiwango cha juu pia lakini sio hao pekee bali ni timu kwa ujumla. Tunatakiwa sasa tujilinda kuanzia katika ushambuliaji hadi katika ulinzi, na tulikuwa na kiwango kizuri hasa katika ulinzi. Tunatakiwa tuendeleze hivi, tushinde mechi zetu na kupigania nafasi nne za juu", ameongeza De Gea.

Katika mchezo huo, David De Gea aliokoa jumla ya michomo 11 ya hatari kutoka kwa Spurs hasa katika kipindi cha pili na kuisaidia timu yake kupata ushindi wa sita mfululizo katika ligi tangu kocha mpya, Ole Gunnar Solskjaer alipoteuliwa mwishoni mwa mwaka uliopita.

Sasa Manchester United imefikisa jumla ya alama 41 sawa na Arsenal iliyo katika nafasi ya tano kwa walama hizo lakini ikiizidi United kwa tofautri ya mabao mawili ya kufunga na kufungwa.