Jumatano , 4th Mei , 2016

Mshambuliaji wa Yanga Donald Ngoma amekiri kwamba mechi ya za nje ya Dar es salaam ni ngumu sana kwake akidai kuwa anakabwa sana na wapinzani huku mabeki wakitumia nguvu nyingi kumzuia.

Ngoma, raia wa Zimbabwe, aliyeifungia Yanga mabao 14, alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana timu yake imekuwa ikipata ushindi mwembamba kila inapocheza nje ya Dar es Salaam.

Ngoma alisema kucheza ugenini hasa mikoani ni ngumu kuchukua pointi tatu kwa maana timu nyingi za huko zimekuwa zikiwakamia kupita kiasi.

Aliongeza kuwa hakuna mchezo wowote rahisi mikoani kwa kuwa wenyeji wamekuwa wakicheza kwa nguvu kuhakikisha wanazibakiza pointi katika uwanja wao na wanapocheza na sisi ndiyo wanaongeza umakini.

Aidha, mchezaji huyo aliendelea kujipa moyo na kusema kitu kikubwa ambacho anafikiria ni kuipa timu yake ubingwa, hivyo watapambana kwa namna yoyote ile na kutumia nguvu za ziada ili kishinda.