Jumatano , 10th Jul , 2019

Timu ya Wanawake (Simba Queens), inatarajiwa kuondoka nchini siku ya Jumatatu Julai 15, 2019 kwenda nchini Ujerumani kwa ziara ya kisoka ya wiki mbili.

Kikosi cha Simba Queens

Msafara wa timu hiyo utakuwa na jumla ya watu 16, wachezaji wakiwa 13 na viongozi watatu, ambapo mkuu wa msafara atakuwa ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Asha Baraka.

Wakiwa nchini humo, wachezaji wa Simba Queens watapata nafasi ya kushiriki semina mbalimbali za kijamii ambazo zina lengo la kuwapa mbinu mbadala za kazi ambazo wanaweza kufanya nje ya maisha ya soka.

Pamoja na hilo pia watacheza michezo minne ya kirafiki, ambapo michezo mitatu itachezwa mjini Hamburg na mwingine mmoja kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Berlin.

Baada ya semina ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa wachezaji wetu na michezo ya kirafiki ambayo itasaidia kuandaa kikosi kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake, msafara wa Simba Queens utarejea nchini siku ya Alhamisi Agosti mosi, 2019.

Safari ya Simba Queens imedhaminiwa na Serikali ya Ujerumani kwa kushirikiana na Simba SC.