Jumanne , 12th Dec , 2017

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amepinga vikali kauli ya kocha Jose Mourinho wa Manchester United kuwa wachezaji wa City walishangalia vibaya mbele yake baada ya ushindi wa jumapili.

Guardiola amesema aliwaambia wachezaji wake washangalie kwasababu walikuwa na furaha na walikuwa na haki ya kufanya hivyo kutokana na aina ya mchezo waliokuwa wameshinda. Manchester City ilishinda 2-1 dhidi ya Man United kwenye dimba la Old Trafford.

“Niliwaambia shangilieni lakini hawakuvuka mipaka wala hawakumlenga mtu yeyote kama Mourinho anavyodai, ilikuwa ni haki yetu kufurahi kwasababu tulishinda mchezo dhidi ya wapinzani wetu wakuu na hata wao wangeshinda wangeshangilia”, amesema Guardiola.

Mourinho alilalamika siku ya jumapili baada ya mchezo kuwa kuwa wachezaji wa Manchester City hawakushangilia vyema na walimvunjia heshima kwa kushangilia kwa aina ya kuzomea.

Hata hivyo Guardiola amesema kama kitendo hicho kilikuwa ni kibaya basi hakitajirudia na wataliandikia shirikisho la soka nchini England (FA) kuelezea ukweli wa tukio hilo.