Guardiola atoa angalizo EPL

Jumatano , 14th Feb , 2018

Baada ya Manchester City kupata ushindi mnono dhidi ya FC Basel kwenye mchezo wa UEFA usiku wa jana kocha Pep Guardiola amesema sasa ni muda wa kuwekeza nguvu kwenye ligi kuu ya England.

Guardiola anaamini kuwa baada ya ushindi wa 4-0 ugenini tayari timu yake imeingiza mguu mmoja katika robo ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hivyo kwasasa hawana budi kujielekeza kwenye mapambano ya kusaka ubingwa wa EPL.

''Niliwaambia wachezaji kuwa tukishinda kwa mabao mengi itatusaidia kucheza mechi za ligi bila presha na vijana wamefanya hivyo kwahiyo tutaweka nguvu zaidi kwenye makombe mengine japo hatuwezi kudharau mechi ya marudiano'', alisema baada ya mchezo.

Mabao ya Manchester City jana yalifungwa na Ilkay Gundogan aliyefunga mawili huku Bernardo Silva na Sergio Aguero wakifunga bao moja hivyo kuipa asilimia kubwa timu hiyo ya kuvuka hatua ya 16.

Manchester City ambayo inaongoza ligi kwa alama 72, itakuwa dimbani kwenye michuano ya FA kuivaa Wigan Athletic wiki ijayo.