Jumatatu , 7th Dec , 2020

Ligi kuu za soka barani ulaya zinatazamiwa kuendelea hii leo kwa michezo kadhaa kupigwa katika madimba mbalimbali.

Mshambuliaji wa Southampton, Dany Ings anayetarajiwa kurejea kikosini leo.

Ligi pendwa Duniani ya nchini Uingereza itaendelea kwa mchezo mmoja, Southampton watakuwa ugenini dhidi ya Brighton & Hove Albion saa 5 kamili usiku.

Brighton wataingia dimbani wakiwa na urejeo wa winga wake machachari na hatari Tariq Lamptey aliyekosekana kwenye mchezo uliopita kwasababu ya kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja kufuatia kuoneshwa kadi nyekundu dhidi ya Aston Villa.

Southampton wanatarajia kukipiga wakiwa na taarifa njema ya kurejea kikosini mshambuliaji wake tegemeo Danny Ings aliyekosekana uwanjani tokea tareje 1 mwezi uliopita kufuatia majeraha aliyoyapata.

Danny Ings amefunga mabao 5 kwenye michezo 7 ya EPL aliyocheza msimu huu, Brighton wanashika nafasi ya 16 wakiwa na alama 10 ilhali Southampton wanashika nafasi ya 8 wakiwa na alama 17.

Nchini Hispania, Valencia inayoshika nafasi ya 16 wakiwa na alama 13 wamesafiri kuwafuata Eibar wanaoshika nafasi ya 13 wakiwa na alama 12 kuwania alama 3 muhimu kwenye mchezo wa ligi kuu nchini humo unaotazamiwa kupigwa saa 5 kamili usiku wa hii leo kwenye dimba la Ipurua.

Huko Ujerumani, kwenye dimba la Prezerio ligi hiyo itaendelea kwa mchezo mmoja ambapo TSG, Hoffenheim inayoshika nafasi ya 13 wakiwa na alama 9 watakuwa wenyeji wa Augsburg waliopo nafasi ya 10 baada ya kujizolea alama 13 mchezo utakaochezwa mishale ya saa 4:45 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Nako nchini Italia, ni vita ya mchezo mmoja kwa timu zilizopo mkiani ambapo Genoa waliopo nafasi ya pili kutoka mwisho wakiwa na alama 5 watapepetuana na Fiorentina wanaoshika nafasi ya 17 wakiwa na alama 8 kwenye dimba la Artemio Franchi, Firenze saa 4:45 usiku kwa saa za kitanzania