Alhamisi , 8th Nov , 2018

Siku moja baada ya uongozi wa KMC kutangaza kuachana na kiungo wao Abdulhalim Humud kutokana na utovu wa nidhamu, nyota huyo ameibuka na kukanusha vikali tuhuma hizo.

Abdulhalim Humud

Mapema wiki hii uongozi wa KMC, kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu Walter Harrison ilitangaza rasmi kuachana na kiungo huyo kutokana na utovu wa nidhamu wakimtuhumu kuwalaghai/kutongoza wanawake wa wachezaji wenzake na kuleta mtafaruku mkubwa kabuni hapo.

Humud amesema suala hilo la yeye na wake wa wachezaji wenzake ni shutuma ambayo KMC wameamua kumtengenezea lakini sio kweli na wala hana tabia hiyo.

"Nilikuwa nje ya nchi na wakati nipo njiani narudi ndio nikakutana na shutuma hizo za uzushi ambazo uongozi wa KMC imenitengenezea," alisema.

Akizungumzia suala la kuvunja mkataba na klabu hiyo Humud amesema aliamua kuuandikia barua uongozi wake kuomba kuachwa kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu na sio vinginevyo.

"Niliandika barua ya kuomba kuachwa baada ya kushauriana na watu wangu wa karibu lakini nilipata majibu ambayo hayakuwa mazuri kutoka kwa viongozi wangu," amesema.