Ijumaa , 24th Jan , 2020

Usiku wa Alhamisi, Januari 23, 2020 Klabu ya Liverpool imeshinda mchezo wake wa 14 mfululizo katika EPL msimu huu ilipoifunga Wolves mabao 2-1 katika uwanja wake wa nyumbani wa Molineux.

Sadio Mane na kocha Jurgen Klopp

Baada ya mchezo huo, sasa Liverpool imefikisha jumla ya pointi 67 baada ya kushuka dimbani michezo 23, ambapo nafasi ya pili inashikiliwa na Manchester City ambayo ina pointi 51 na nafasi ya tatu ni Leicester City yenye pointi 48.

Mapema kipindi cha pili, Liverpool ilipata pigo baada ya mshambuliaji Sadio Mane kuumia, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na kiungo mpya aliyesajiliwa dirisha hili dogo, Takumi Minamino.

Jeraha la Mane limeamsha wasiwasi ndani ya klabu hiyo juu ya muendelezo wake wa ushindi na kutopoteza mechi ikiwa katika mbio za kuufukuzia ubingwa wa kwanza wa ligi tangu miaka 30 iliyopita. Kocha wa klabu hiyo Jurgen Klopp amezungumzia juu ya jeraha lilo la mshambuliaji wake akisema kuwa ni maumivu tu ya mguu.

"Hatujajua shida ni nini ni misuli. Alihisi kitu kwenye msuli. Hatujui bado, ni wazi lazima tungojee. Tutaona", amesema Klopp.

Mane ameonekana kuwa na msaada mkubwa katika klabu ya Liverpool msimu huu, akiongoza kwa ufungaji kwenye klabu hiyo kwa mabao 11, akitoa assist 6 na uwiano wa goli kila mechi ni 0.5, kitu ambacho kinaleta maswali endapo atakosekana kwa michezo mingi ijayo.