Ijumaa , 17th Jul , 2015

Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi hapo kesho kwa kuzikutanisha timu za Yanga ikimenyana na Gorhamia uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Baraza la vyama vya soka kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA, Nicholaus Musonye amesema, mechi dhidi ya Yanga na Gor mahia itatanguliwa na mechi ya APR ya Rwanda wakikutana na Al-Shandy ya Sudan saa nane mchana huku KMKM ikichuana na Telecom Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Kwa upande wa Kocha mkuu wa Yanga Hans Van Pluijm amesema, anawaheshimu sana wapinzani wake timu ya Gor Mahia lakini hawaogopi na anamatumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

Pluijm amesema, wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuikabili kila timu kwenye michuano hiyo ambapo kitu kikubwa huwa hadharau wapinzani kwasababu kwenye soka lolote linaweza kutokea na hakuna mtu anayejua matokeo.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Gor Mahia, Frank Nuttal amesema yeye hana uzoefu mkubwa kwenye soka la Afrika ukilinganisha na mpinzani wake ) lakini vijana wake wako vizuri kuikabili Yanga kesho kwenye uwanja wa Taifa.

Nuttal amesema, Yanga ni timu kubwa japo hajawahi kuiona ikicheza lakini anaamini ni timu yenye ushindani na mechi ya kesho itakuwa ngumu lakini mwisho wa mchezo watajua matokeo.

Kwa upande wa Kocha msaidizi wa APR ya Rwanda Mashime Vicent ambayo itakutana na Al-Shandy ya Sudan amesema, timu yake ipo vizuri na wamejipanga kuchukua Ubingwa kwani mwaka jana ilimaliza michuano hiyo ikiwa na El Merreikh ya Sudan lakini haikufanikiwa kuchukua Ubingwa.

Mashime amesema, wachezaji katika kikosi chake ni vijana ambao anaamini watafanya vizuri katika michuano hiyo.