Jumamosi , 24th Oct , 2020

Nahodha wa timu ya Yanga, Lamine Moro ameweka wazi kuwa mchezo wa kesho wa ligi dhidi ya KMC utakaochezwa katika uwanja wa CCM Kirumba utakuwa mgumu lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata alama zote tatu.

Nahodha wa Yanga, Lamine Moro akiwa katika moja ya mchezo wa klabu yake.

Kikosi cha Yanga kikiongozwa na Mwenyekiti wake Dk. Mshindo Msola tayari kimetua jijini Mwanza asubuhi ya leo tayari kwa ajili ya mchezo huo unao subiriwa kwa hamu.

Lamine amesema kila mechi wanaipa umuhimu sawa na hawadharau timu yoyote ndio maana wanapambana kwenye kila mchezo ili kupata alama tatu.

Mchezo wa kesho utakuwa ni wa pili kusimamiwa na kocha Cedric Kaze tangu alipochukua nafasi ya Zlatico Krmpotic ambapo mechi yake ya kwanza ilikuwa siku ya Alhamisi dhidi ya Polisi Tanzania na kufanikiwa kupata ushindi wa bao moja.

Baada ya mchezo wa kesho mabingwa hao mara 27 wa ligi kuu wataendelea kusalia Kanda ya Ziwa ambapo wiki ijayo watacheza na Biashara United mkoani Mara.

 

Ikumbukwe katika msimu uliopita, Yanga ilishindwa kuifunga KMC, baada ya kupoteza mchezo mmoja na sare moja katika ligi kuu Tanzania bara.