Klopp aomba msamaha kiaina Camp Nou

Jumatano , 1st Mei , 2019

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ameonesha kutofurahishwa na namna waandishi wa habari walivyomnukuu juu ya kauli yake kuhusu uwanja wa Barcelona, Camp Nou.

Kocha Jurgen Klopp

Klopp amesema kuwa wanahabari wameandika habari potofu juu ya kauli yake aliyozungumzia uwanja wa Camp Nou, alipoulizwa maoni yake kufuatia kurasa za mitandao ya kijamii za Barcelona kupost video iliyoambatana na maneno, "nyumbani kwetu, hekalu letu, ngome yetu".

Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Klabu Bingwa Ulaya kati ya FC Barcelona na Liverpool katika dimba la Camp Nou, usiku wa leo, Klopp amesema, "haikuwa ni kwaajili ya kudharau kwasababu Barcelona walikuwa wakitawala, ilikuwa ni muhimu kwa timu kufahamu kuwa ilikuwa ni uwanja wa kawaida na sio hekalu, ngome au kitu kingine", amesema.

"Ninaongea vitu 500,000 vya msingi kuhusu Barcelona, mnajaribu kucheza mchezo kwa kubadilisha maneno na kuyafanya mambo kuwa makubwa, mimi ni shabiki wa soka kwa muda mrefu kuliko hata kazi yangu ya ukocha, mnafikiri nitasema nini kibaya kuhusu uwanja huu?".

Barcelona itakutana na Liverpool usiku wa leo, huku Liverpool ikiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza mechi nne za ugenini dhidi ya Barcelona, ikishinda mechi mbili na kutoka sare mechi mbili. Barcelona pia imeshinda mechi nyingi zaidi (27) dhidi ya timu za Uingereza, kuliko timu nyingine yoyote ya nje ya Uingereza katika michuano ya Ulaya.

Pia akimzungumzia kiungo wa Barcelona, Phillipe Coutinho, kocha Jurgen Klopp amesema kuwa alipenda kufanya kazi na mchezaji huyo kwa saababu ni mchezaji bora wa kiwango cha Dunia na aliposikia kwa mara ya kwanza kuwa anataka kwenda Barcelona alikuwa akiwaza timu yake ambavyo itacheza bila ya uwepo wake.