Jumanne , 2nd Feb , 2021

Mabingwa wa ligi kuu Engalnd klabu ya Liverpool imefanya usajili wa mabeki wawili wa kati, Ozak Kabak na Ben Davies, masaa machache kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa jana usiku , lakini pia klabu hiyo itakosa huduma ya Joel Matip msimu mzima.

Liverpool wametumia zaidi ya Biolioni 6 za kitanzania kukamilisha usajili wa Ben Davies

Taarifa za usajili wa walinzi wapya wa Liverpool ziliambatana na taarifa za majeruhi ya mlinzi Joel Matip kuwa atakuwa nje ya uwanja kwa michezo yote iliyosalia ya msimu huu kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu aliyopata kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tottenham ambapo Majogoo walishinda kwa mabao 3-1.

Ozak Kabak Raia wa Uturuki mwenye umri wa miaka 20 amajiunga na Liverpool kwa mkataba wa mkopo mpaka mwishoni mwa msimu akitokea Schalke 04 ya Ujerumani,lakini pia mkataba huo una kipengele cha majogoo hao wa jiji la Liverpool kumnunua mchezaji huyo kama wakiridhishwa na kiwango chake, Ben Davies anajiunga na Liverppol akitokea Preston North End ya Nchini England kwa ada ya uhamisho ya fedha za Uingereza pauni million 2 ambayo ni zaidi ya billion 6 za kitanzania.

Usajili wa walinzi hawa ulikuwa hauepukiki kwa kocha Jurgen Klopp mara baada ya taarifa za Matip kuwa atakuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima, hivyo kocha huyo Mjerumani anawakosa walinzi wake wake wa kati watatu kufuatia majeruhi ya muda mrefu yaani Virgil van Dijk na Joe Gomez ambao nao kuna uwezekano mkubwa wasicheze tena msimu huu kutokana na majeruhi.

lakini pia Klabu ya Liverpool imemtoa kwa mkopo Mshambuliaji wake Takumi Minamino kwenda klabu ya Southampton mpaka mwishoni mwa msimu.

Na kwingineko baadhi ya sajili ambazo zilikamilika usiku wa jana kabla ya dirisha kufungwa ni pamoja na mshambuliaji Joshua King amejiunga na Everton akitokea Bournemouth, Southampton imemtoa kwa mkopo mshambuliaji wake Shane Long kwenda Bournemouth, na washika bunduki wa London Arsenal imewatoa kwa mkopo kiungo Joe Willock kwenda Newcastle United, Ainsley Maitland-Niles nae kajiunga na West Brom wakati mlinzi Shkodran Mustafi kasaini Schalke 04.