
Joe Allen akipiga penati ya mwisho iliyoipeleka Liverpool fainali ya Capital One Cup usiku wa jana uwanja wa Anfield
Liverpool inaelekea Wembley kwa mara nyingine baada kuiondosha Stoke City kwa mikwaju ya penati 6-5, kwenye nusu fainali ya pili kombe la Capital One usiku wa jana uwanja wa Anfield.
Joe Allen na Simon Mignolet walikuwa mashujaa wa Liverpool kwenye usiku huo, lakini kocha wa timu hiyo Jurgen Klopp amesema hakuona penati zikipigwa kwa sababu alikaa chini ili asiwazibe wapenzi wa timu hiyo waliokuwa nyuma jukwaani.
Klopp amesema"Nilitaka kuzitazama (penati) lakini watu kwenye viti vya mbele walinambia wasingeweza kuona kwa sababu mimi ni mrefu. Kwahiyo nilikaa kiti cha mbele na sikuweza kuona".
Allen aliyeingia kipindi cha lala salama katika muda wa kawaida, alipiga penati ya mwisho iliyowapeleaka majogoo hao fainali, kabla ya mlinda mlango Mignolet kufuta penati mbili za Marc Muniesa na Peter Crouch.
Marko Arnautovic aliifungia Stoke muda mfupi kabla ya kwenda mapumziko na kufanya matokeo yawe 1-1 kufuatia Liverpool kushinda mchezo wa kwanza bao 1-0 na hadi dakika 90 zinakamilika matokeo yalikuwa sare ya 1-1,ndipo mchezo ulipoenda muda wa ziada lakini hakukuwa na mabao mengine na kufuata tukio la penati.
Majogoo wa jiji, Liverpool sasa wanasubiri kucheza fainali na mshindi wa mchezo wa leo usiku kati ya Everton na Manchester City, Februari 28 uwanja wa Wembley.