Jumatano , 14th Apr , 2021

Majogoo wa jiji, klabu ya Liverpool wanakibarua kizito cha kupindua matokeo kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid saa 4:00 usiku wa leo Aprili 14, 2021 baada ya kufungwa mabao 3-2 kwenye mchezo mkondo wa kwanza.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp (kushoto) na kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane (kulia).

Kuelekea kwenye mchezo huo, kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amesema licha ya kuwa walifanikiwa kupindua meza miaka miwili iliyopita kwa kupata ushindi wa mabao 4-0 Anfield walipofungwa mabao 3-0 Camp Nou dhidi ya Barcelona na kutinga fainali na kuwa mabingwa.

Klopp amesema, “Ukiwa nyuma kwa mabao 3-1, inaonekana tayari umetolewa. Tutajaribu kupindua matokeo. Haupindui matokeo kwasababu ulipindua matokeo kipindi cha nyuma. Utapata nafasi pekee kama ukicheza mchezo mzuri kwa wakati uliopo”.

Kujibia kucheza bila mashabiki ambao uwepo wao ni silaha kwa hamasa ya Liverpool kwenye uwanja wa Anfield, Klopp amesema “Litakuwa suala gumu tena bila mashabiki uwanjani, tunapaswa kujitengenezea mazingira hayo sisi wenyewe kwenye mchezo huu na tutafanya hivyo”

Hii itakuwa inatazamiwa kuwa ni kwa mara ya tatu, Real Madrid kucheza Anfield na michezo yake miwili iliyopita alipata kipigo mchezo mmoja, mwaka 2009 kwa kufungwa mabao 4-0 na kupata ushindi mchezo mmoja, mwaka 2014 wa mabao 3-0.

Liverpool wanatazamiwa kumjumuisha kikosini kiungo wake, Curtis Jones kuchukua nafasi ya Naby Keita aliyeshindwa kuonesha cheche mchezo uliopita na ilhali Real Madrid wanatazamiwa kumkosa Lucas Vazques aliyepata majeraha juma lililopita.

Wachezaji waliopata majeraha ya muda mrefu, Nahodha wa Liverpool, Jordan Henderson bado hana uhakika wakurejea usiku wa leo huku Eden Hazard mwenye majeraha na Sergio Ramos na Rafael Varane wamekutwa na maambukizi ya Covid-19.