Alhamisi , 18th Apr , 2019

Baada ya kupoteza mchezo wa pili mfululizo wa michuano ya vijana chini ya miaka 17 ya AFCON inayoendelea nchini, kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo amesema haoni sababu ya kung'atuka katika timu hiyo.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo

Jana, April 17, Serengeti Boys imepoteza mchezo wa pili mfululizo dhidi ya Uganda na kupelekea kufifisha matumaini ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia ya Vijana chini ya miaka 17, itakayofanyika nchini Brazil.

Mirambo amesema kuwa haoni sababu ya kung'atuka kuifundisha Serengeti Boys kwasababu vijana hao wamewekewa mipango ya kukuzwa na itaendelea kama kawaida kwa mashindano yajayo.

"Kuhusu kama nimeshindwa kuipeleka timu katika fainali za Kombe la Dunia niachie nafasi hii sidhani kama litakuwa jambo sahihi kwa maana nitakuwa nakimbia changamoto. Timu ina mipango na mashindano yanaendelea, ninaweza kuamua kung'atuka lakini ni kwa mustakabali wa nani," alisema Mirambo.

Serengeti walifungwa mechi ya kwanza na Nigeria kwa mabao 5-4, na katika mchezo dhidi ya Uganda wakakubali tena kichapo cha mabao 3-0, ambapo sasa inasubiri kumalizia mchezo wa mwisho katika kundi lao dhidi ya Angola.

Mpaka sasa timu zilizojihakikishia nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia la vijana ni timu za vijana za Cameroon na Nigeria.