Jumatatu , 27th Jan , 2020

Kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Luc Eymael amesema kuwa hapendi kuona mchezaji wake mpya, kiungo Bernard Morrison akiwadhalilisha wapinzani wake kwa staili yake ya uchezaji.

Bernard Morrison na kocha Luc Eymael

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho 'Azam Sports Federation Cup (ASFC)' dhidi ya Tanzania Prisons Jumapili, Januari 26 na kushinda 2-0, kocha Eymael amesema kuwa ameshaoongea na mchezaji huyo juu ya aina yake ya mchezo ambao unawadhalilisha wapinzani.

"Mimi sipendezwi kuona mtu anawadhalilisha wengine, ukifanya vile Ulaya utafanyiwa 'tackle' ya hatari sana. Ukiangalia Liverpool, Mo Salah anaweza kufanya hivi?, Sadio Mane anafanya hivi? hapana na mimi nimeshaongea na Morrison nimemwambia sipendi staili hii", amesema Eymael.

"Mashabiki wanapenda kuona mchezaji akifanya hivyo lakini kwangu mimi ni kutowaheshimu wapinzani na nimeshamwambia Bernard Morrison", ameongeza.

Morrison ameibukia kupendwa na mashabiki wa Yanga siku za karibuni kutokana na staili yake ya kuchezea mpira kwa madaha, ikiwa ni pamoja na kusimama juu ya mpira, huku akionesha kiwango bora uwanjani.