Jumamosi , 18th Jun , 2016

Timu ya Taifa ya mchezo wa Kriketi ya Tanzania inataraji kuingia kambini rasmi hii leo jijini Dar es Salaam tayari kuanza mazoezi ya mawindo kwaajili ya michuano ya kimataifa ya Afrika itakayofanyika mwezi wa Septemban nchini Afrika kusini.

Baadhi ya wachezaji wa Kliketi wakichuana katika moja ya mechi za mchezo huo.

Timu hiyo inaingia kambini kwa mazoezi katika viwanja vya chuo kikuu cha Dar es Salaam ili kujiwinda na mashindano ya kimataifa ya kombe la Afrika ambayo yatafanyika kuanzia Septemba 11- 19 mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Mratibu wa timu hiyo ya Taifa na mkuu wa kamati ya ufundi wa chama cha mchezo wa kriketi nchini Tanzania TCA ambaye ni kocha na mchezaji wa mchezo huo Hamis Abdalah amesema maandalizi yote ya kambi hiyo yamekamilika na wanataraji zaidi ya wachezaji 30 wataingia kambini kwaajili ya maandalizi hayo.

Abdalah amesema wameamua kuanza kambi mapema ili kuwapa nafasi ya kutosha wachezaji wakutoka mikoani na wahapa waweze kujiandaa vema na kuzoeana ili kujenda timu imara na baadae waweze kupata kikosi bora ambacho kitakuwa kimefanya mazoezi ya kutosha na kuzoeana na kwenda katika mashindano hayo kushindana na kutoa upinzani wa kutosha.

Aidha Abdalah amesema katika kikosi hicho kamati ya ufundi ya TCA imewapa fursa vijana chipukizi kujifunza mbinu mbalimbali za mchezo huo kwakuwachanganya na wale wenye uzoefu kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini hasa katika mikoa ambayo inafaya vema katika mchezo huo kama Arusha, Mwanza, Morogoro, Tanga na Dar es Salaam.

Akimalizia Abdalah ametoa wito kwa Watanzania kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya maaandalizi mazuri na kuiwezesha kwenda kushindana na hatimaye kuibuka na ubingwa wa kombe hilo la Afrika.