Jumatatu , 9th Mei , 2022

Vinara wa Ligi Kuu soka Tanzania bara NBC Premier League Yanga SC wanashuka dimbani leo saa 1:00 usiku kucheza dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Benjamini Mkapa. Ukiwa ni mchezo pekee unaochezwa leo.

Yanga haijafungwa mchezo hata mmoja msimu huu wa 2021-22 kwenye Ligi Kuu Tanzania bara

Kocha mkuu wa timu ya wananchi Yanga SC Nasreddine Nabi anarejea leo kwenye benchi la ufundi baada ya kukosa michezo 3 iliyopita ambayo alikuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa kutokana na utovu wa nidhamu.

Yanga ndio vinara wanaongoza Ligi kwa tofauti ya alama 10 wakiwa na alama 56, na Simba SC walionafasi ya pili wana alama 46. Timu ya wananchi haijashinda michezo miwili mfululizo iliyopita ambayo yote walitoka suluhu dhidi ya Simba na Ruvu Shooting na kuelekea mchezo huu kocha Nabi amesema kama wanataka ubingwa basi wanahitaji alama zote 3 kwenye michezo yote iliyosalia.

Tanzania Prisons wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa wametoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Mbeya kwanza kwa bao 1-0, na kwenye msimamo wa Ligi wapo nafasi ya 15 wakiwa na alama 22. Kwenye michezo 5 ya mwisho wameshinda 3 na wamefungwa michezo 2.

Rekodi kwenye mchezo huu zinaibeba Yanga mbele ya Tanzania Prisona kwani katika michezo 5 ya mwisho kukutana kwenye Ligi Kuu Yanga wameshinda mara 2 na michezo 3 imeisha kwa sare. Na mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu Yanga ilishinda kwa mabao 2-0. Huu ni mchezo pekee wa ligi Kuu unaochezwa leo na ni wa raundi ya 23 kwa timu zote mbili.