Ijumaa , 23rd Mar , 2018

Baada ya droo yao kutoka na kupangiwa timu ya Welayta Dicha F.C ya Ethiopia, kocha mkuu wa mabingwa wa soka nchini Yanga George Lwandamina, amesema timu hiyo sio njia ya mkato kwa Yanga kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kwa kufikiria ni timu kutoka Ethiopia tunaweza kuitoa ni sawa, lakini tukumbuke ratiba yetu yote msimu huu ilikuwa rahisi kwa kufikiria na tumekumbana na upinzani wa hali ya juu hivyo hatutawabeza wapinzani wetu na tutajiandaa kwaajili ya kuvuka na kuingia makundi'', amesema.

Kauli ya Lwandamina imekuja ikiwa ni muda mfupi baada ya tarehe ya mchezo wao kutangazwa ambapo Yanga itakuwa uwanjani tarehe 7/4/2018 kucheza dhidi ya Welayta Dicha.

Kabla ya mchezo huo Yanga itacheza mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida United. Mchezo huo utachezawa April 1 kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida ikiwa ni mchezo wa robo fainali.