Ijumaa , 13th Nov , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ameitakia kheri, timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars katika mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu fainali za AFCON mwaka 2021 dhidi ya Tunisia leo usiku.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt.John Pombe Magufuli ameitakia kheri Taifa Stars kwenye mchezo dhidi ya Tunisia leo usiku

Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Bungeni Jijini Dodoma katika hotuba yake ya ufunguzi rasmi wa bunge la 12, ambapo amesema kwamba Watanzania wanataka ushindi hivyo basi Taifa Stars inapaswa kushinda hii leo.

Taifa Stars ilifanya mazoezi ya mwisho jana usiku kabla ya mchezo wa usiku wa leo na hakuna mchezaji mwenye majeruhi zaidi ya nahodha Mbwana Samatta, ambaye atakosekana, kutokana na majeruhi ambayo yatamfanya akose mechi ya marudiano inayotarajiwa kuchezwa Novemba 17, 2020, Jijini Dare s salaam.

Tunisia imeshinda michezo yake yote miwili na wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa ndio vinara wa kundi J wakiwa na alama 6, ikiwa ni tofauti ya alama 3 na Tanzania yenye alama 3 na inaburuza mkia kwenye kundi hilo.

Alama hizo 3 taifa Stars ilizipata baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Equatorial Guinea, kwa ushindi wa magoli 2-1, na mchezo wa pili walipoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Libya.

Tunisia ilizifunga Libya mabao 4-1 na Equatorial Guinea bao 1-0. Kwenye msimamo wa kundi hilo Tunisia wanaongoza nafasi ya pili wapo Equatorial Guinea na alama 3 Libya wapo nafasi ya 3 wakiwa na alama 3, na Tanznaia ndio wanaoburuza mkia.

Huu ni mchezo wa kihistoria kwani ni kwa mara ya kwanza mataifa haya yanakutana, timu hizi hazikuwahi kukutana kwenye mashindano yoyote hapo awali.