Jumanne , 25th Mar , 2014

Timu za Azam na Yanga ambazo zinachuana kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara (VPL) zinashuka tena viwanjani kesho kuwania pointi tatu.

Azam yenye pointi 47 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya mabingwa watetezi Yanga na Tanzania Prisons kuanzia saa 10.30 jioni.

Kwa upande mwingine Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea amri ya Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) kukamata sh. milioni 106 za klabu ya Yanga kutokana na mapato ya mlangoni kwenye mechi zake ili kuwalipa waliokuwa wachezaji wake Stephen Malashi na Wisdom Ndlovu.

Afisa haabri wa TFF Boniface Wambura amesema kuwa wachezaji hao walifungua kesi kortini kupinga mikataba yao na klabu hiyo kuvunjwa bila kulipwa haki zao za kimkataba. Malashi na Ndlovu walishinda kesi hiyo, hivyo korti kuwapa tuzo hiyo ya sh. milioni 106 na wao kama TFF kazi yao ni kutekeleza amri hiyo.