Manara amvaa tena Nugaz, ni kuhusu lugha

Ijumaa , 17th Jan , 2020

Mnyukano wa maneno unaendelea kati ya Afisa Habari wa Simba, Haji Manara na Afisa Mhamasishaji na Msemaji wa Yanga, Antonio Nugaz huku kila mmoja akijaribu kuisimamisha timu yake.

Haji Manara na Antonio Nugaz

Hali hiyo imekuwa ikionekana katika mitandao ya kijamii na hata katika mahojiano yao mbalimbali na vyombo vya habari, na kuleta mijadala mbalimbali miongoni mwa mashabiki wa timu hizo.

Hivi karibuni baada ya kumalizika kwa mchezo wa Yanga na Kagera Sugar na kushuhudia Yanga ikifungwa 3-0 nyumbani, Antonio Nugaz alikaririwa akisema kuwa walishindwa wenyewe kutumia nafasi walizozitengeneza, ambapo hii leo Haji Manara ameibuka na kukosoa lugha aliyotumia katika maelezo yake.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Manara amezungumzia kauli ya Nugaz kwa utani akisema, "rafiki yangu mimi huyo, eti ku'compose', najua alikusudia ku'convert', sitachoka kumweka sawa, mzigo wangu mwenyewe huu, halafu sasa hivi nishaanza kumfundisha kuongea kwa authority, sio hyo staili yake, huku kwenye soka ukiongea Mwamba wa Pua unaukaza kidogo, hii yaani huku sio, watu wa huku hovyo kidogo".

Tambo za maafisa hao zimeanza kuelekea kwenye mchezo wao uliopigwa wiki mbili zilizopita ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, huku ushujaa ukionekana kwa Yanga ambao waliamka na kusawazisha mabao yote mawili ndani ya dakika 10 za kipindi cha pili cha mchezo.