Jumatatu , 21st Jan , 2019

Klabu ya soka ya Simba imerejea asubuhi ya leo kutokea mjini Kinshasa ambako ilicheza mchezo wa Klabu Bingwa Barani Afrika dhidi ya AS Vita Club.

Haji Manara

Simba imereja nyumbani ikiwa na kumbukumbu mbaya kichwani, ikipoteza mchezo huo kwa mabao 5-0.

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara ambaye amekuwa akiandamwa na mashabiki wa Yanga kutokana na tambo zake, amejitokeza na kueleza sababu ambayo imepelekea ukimya wake baada ya mchezo huo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Manara amesema kuwa sababu iliyomfanya kushindwa kujibu ujumbe wa watani wake ni tatizo la mtandao nchini DR Congo.

 

Kufuatia matokeo hayo, sasa Simba inakamata nafasi ya tatu katika kundi lake la D, ikiwa na alama 3 na magoli 3. Kundi hilo linaongozwa na Al Ahly iliyo na alama 4, AS Vita iliyo nafasi ya pili kwa alama 3 na JS Saoura inayoburuza mkia kwa alama moja pekee.

Baada ya kurejea nchini, Simba itaingia moja kwa moja kambini tayari kwa maandalizi ya mashindano ya Sport Pesa Seper Cup yanayotarajia kuanza kesho katika uwanja wa taifa, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya klabu hiyo.

Simba inatarajia kukutana na AFC Leopards ya Kenya katika mchezo wa awali na imesema kuwa itayatumia mashindano hayo kwaajili ya kujiandaa na michuano inayoendelea ya Klabu Bingwa Afrika.