Manara awataka wachezaji kuchukua tahadhari

Alhamisi , 16th Mei , 2019

Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara amewakumbusha wachezaji wa klabu hiyo siri ya mafanikio kuelekea katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar hii leo.

Wachezaji wa Simba

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Manara amezungumzia umuhimu wa mchezo huo dhidi ya Mtibwa, akiufananisha na mchezo wa hatua ya 16 bora ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya AS Vita jijini Dar es salaam, ambapo amewakumbusha jinsi walivyohamasishana katika chumba cha kubadilishia nguo.

"Wachezaji wetu wapendwa, mnajua mapenzi waliyonayo Wanasimba kwenu, mnafahamu kiu yao!!, mnajua karaha wazipatazo mtaani msiposhinda mabingwa wetu wa nchi!!, najua sometimes mpira una matokeo ya kihayawani lakini nyie ni 'another level' mkidhamiria kwa jinsi nnavyowajua", amesema Manara.

"Nakumbuka mlipoambiana 'Dressing room' katika mchezo na As Vita, hebu katupeni pointi tatu leo!!, tunahitaji pointi tatu tu vijana wetu, Yes Mtibwa ni timu bora mno ila mkiamua kwa uwezo wa Mungu, nyie ni bora maradufu".

"Haya haya haya haya wanaume, Wanasimba leo watakuja kuwapa support ili tuanike makopa juani!, inshaallah kheri", ameongeza.

Simba iko katika nafasi ya pili kwa pointi 82, nyuma ya Yanga iliyo katika nafasi ya kwanza kwa pointi 83. Ratiba ya ligi kuu inatarajia kumalizika Mei 28 kwa timu zote kushuka dimbani katika viwanja tofauti tofauti.